--- title: "Kiambatisho cha Usimamizi v1.2" slug: "management-annex-v1-2-swahili" status: "new" updated: 2026-11-20T12:00:06Z published: 2026-11-20T12:00:06Z canonical: "knowledge.rainforest-alliance.org/management-annex-v1-2-swahili" --- > ## Documentation Index > Fetch the complete documentation index at: https://knowledge.rainforest-alliance.org/llms.txt > Use this file to discover all available pages before exploring further. # Kiambatisho cha Usimamizi v1.2 ![](https://cdn.document360.io/929f3fed-0f9d-454a-80e4-d7496bf45e88/Images/Documentation/indicator-guidance-image-g96v93xw.png?sv=2026-02-06&spr=https&st=2026-11-20T20%3A47%3A28Z&se=2026-11-20T21%3A47%3A28Z&sr=b&sp=r&sig=5lONWbMTsk%2BI%2BMQcC1cS%2BptAhpnMYiIQior4nJbZWXE%3D) | Kichwa: | Kiambatisho cha Usimamizi | | --- | --- | | Msimbo: | A-04-SCRL-B-CH | | Toleo: | 1.2 | | Inatumika kwa: | Wamiliki wa Vyeti vya Shamba | | Utekelezaji: | Maudhui ya kuunganisha | | Kuanzia: | Machi 1, 2026 | | Inakamilika ifikapo: | Hadi itakapotangazwa vinginevyo | | Imechapishwa mnamo: | Septemba 17, 2025 | | Imeunganishwa na: | [A-1-S-B-F-V1.4 Kiwango cha Kilimo Endelevu cha shirika la Rainforest Alliance.](https://knowledge.rainforest-alliance.org/docs/rainforest-alliance-sustainable-agriculture-standard-farm-requirements-swahili) [A-33-R-B-FA-V1.0 Kiwango cha Kilimo Rejelevu cha shirika la Rainforest Alliance.](https://knowledge.rainforest-alliance.org/docs/rainforest-alliance-regenerative-agriculture-standard-swahili) | | Inachukua nafasi ya: | [A-04-SCRL-B-CH-V1.1 Kiambatisho cha Usimamizi](https://knowledge.rainforest-alliance.org/docs/management-annex) | ### Hati hii inahusu nini? Kiambatisho hiki kinajumuisha maudhui ya ziada ya lazima yanayohusiana na utekelezaji wa Mahitaji katika Sura ya Usimamizi ya Viwango vya shirika la Rainforest Alliance. Hati hii inajumuisha: - Maelezo ya ziada kuhusu mahitaji ya msingi 1.2.10 na 1.2.11 yanayohusu ukusanyaji wa data ya eneo la kijiografia. - Maelezo ya ziada kuhusu hitaji la msingi 1.3.3 linalohusu mafunzo ya wakaguzi wa ndani. - Maelezo ya ziada kuhusu hitaji la msingi 1.4.1 linalohusu ukaguzi wa ndani. - Ufafanuzi kuhusu utekelezwaji wa mahitaji ya msingi 1.1.1 na 1.4.3. ### Lini na jinsi ya kutumia hati hii? Hati hii inawapa Wamiliki wa Vyeti na Mashirika ya Uidhinishaji maelezo ya ziada kuhusu mahitaji ya msingi yaliyojumuishwa katika viwango vya shirika la Rainforest Alliance. ## Mabadiliko katika toleo lililosasishwa kutoka v1.1 hadi v1.2 | **Sehemu** | **Nini kimebadilika** | | --- | --- | | Katika hati nzima | Ongezo la Kiwango cha Kilimo Rejelevu cha shirika la Rainforest Alliance. | | 1. Ukusanyaji Data za Eneo la Kijiografia | Jedwali la mfano limeondolewa na maandishi yamebadilishwa kwa ajili ya uwazi. | | 3. Ufafanuzi | Sehemu imeongezwa ili kutoa ufafanuzi kuhusu marejeleo ya Kiwango cha Kilimo Rejelevu katika mahitaji ya msingi 1.1.1 na 1.4.3. | ## 1. Ukusanyaji Data za Eneo la Kijiografia ### 1.1 Utangulizi Kama ilivyoainishwa katika mahitaji ya 1.2.10 na 1.2.11 ya Viwango vya shirika la Rainforest Alliance, Wamiliki wa Vyeti wanapaswa kuwasilisha data ya eneo la kijiografia kwenye jukwaa la shirika la Rainforest Alliance. Sehemu hii ina maelezo ya ziada kuhusu kuzingatia mahitaji haya. ### 1.2 Mahitaji ya Ukusanyaji wa Data za Eneo la Kijiografia Wamiliki wa Vyeti wana wajibu wa kutoa data za eneo la kijiografia za vitengo vyote vya mashamba katika mfumo wa alama ya eneo na poligoni. Vitengo vya mashamba vinaweza kuwa katika umbali mbalimbali kutoka kwa kila kimoja na sio lazima viwe vimepakana. Sehemu za 1.3 na 1.4 zinaeleza kwa muhtasari mbinu ambazo Wamiliki wa Vyeti wanaweza kutumia kukusanya alama za eneo na poligoni. Data ya eneo la kijiografia lazima zitimize mahitaji yote ya muundo yaliyoainishwa katika hati hii kabla ya kupakiwa kwenye jukwaa la Uidhinishaji la shirika la Rainforest Alliance. ### 1.3 Alama za eneo Alama za eneo lazima zikusanywe kama ifuatavyo: 1. Viwianishi lazima vichukuliwe karibu iwezekanavyo na katikati ya shamba/kitengo cha shamba, kwa kuzingatia hali za ndani za shamba (mf. miamba mirefu, mito, ardhi isiyo ya kawaida na hatari). 2. Eneo la alama lazima liwekwe ishara na mtu anayechukua viwianishi (mf. kuweka kijiti ardhini, kuweka alama kwenye mti wa karibu, nk.). Hii ni ili kuhakikisha kuwa eneo lile lile linatumika na wakaguzi wa ndani au wakaguzi wa nje kwa ajili ya kuthibitisha data. 3. Viwianishi vya latitudo na longitudo lazima viripotiwe kwa usahihi: 1. Viwianishi vya latitudo na longitudo lazima vikusanywe kwa kutumia Mfumo wa sasa wa Geodetic (Datum: WGS 84 – Msimbo: EPSG: 4326 2. Katika muundo wa namba, ulio na thamani za nambari pekee. Alama kama vile ishara ya digrii (°) haziruhusiwi. 3. Katika mfumo wa viwianishi vya desimali za digrii (muundo wa DD) 4. Kwa angalau desimali 4 (yaani, Latitudo 9.7611; Longitudo –84.1872). 5. Zikiwa na thamani chanya na hasi zilizo sahihi. Alama katika nusutufe ya kusini zina latitudo hasi, na alama katika nusutufe ya kaskazini zina latitudo chanya. Alama katika nusutufe ya magharibi zina longitudo hasi, na alama katika nusutufe ya mashariki zina longitudo chanya. Hata hivyo, sio lazima kujumuisha alama ya “+”, alama hasi pekee “- “(k.m. latitudo: 9.7611; longitudo: -84.1872). 4. Kurekodi kwa kubadilisha nafasi za thamani za latitudo na longitudo kunapaswa kuepukwa. 5. Viwianishi lazima viwasilishwe kwenye Jukwaa la shirika la Rainforest Alliance au zana nyingine yoyote iliyoainishwa na shirika la Rainforest Alliance, kwa kutumia violezo vinavyohitajika na shirika la Rainforest Alliance. 6. Kila alama ya data ya kitengo cha shamba iliyowasilishwa kwenye jukwaa hili lazima iwe na kitambulisho cha kipekee cha kitengo cha shamba (Farm Unit ID). ### 1.4 Poligoni Kila poligoni ya kitengo cha shamba inayowasilishwa kwenye jukwaa la uidhinishaji la shirika la Rainforest Alliance lazima iwe na kitambulisho cha kipekee cha kipande cha shamba (Farm Unit ID). Wamiliki wa Vyeti wanaweza kukusanya poligoni kwa kutumia mojawapo ya mbinu mbili zilizobainishwa hapa chini. Kwa maelekezo ya kina, angalia Mwongozo D wa shirika la Rainforest Alliance kuhusu data za eneo la kijiografia na ramani za hatari. #### 1.4.1 Poligoni kulingana na alama za marejeleo za eneo Alama zote za marejeleo kwa ajili ya data za poligoni lazima zikusanywe shambani. Data za poligoni zinazotokana na ramani ya karatasi au ya kidijitali pekee sio sahihi na, kwa hivyo, haikubaliki. Baada ya kukusanya alama za marejeleo za poligoni shambani, poligoni inaweza kuundwa kwa kutumia programu ya GIS au zana zinazofanana. #### 1.4.2 Poligoni zilizokusanywa shambani Poligoni za mipaka ya mashamba zilizokusanywa shambani zinapaswa kukaguliwa kwa kutumia programu za GIS, kama vile QGIS, Google My Maps, au Google Earth Pro, ili kubaini na kurekebisha kasoro au kutofautiana kwa taarifa. Nyaraka za mwongozo zenye maelezo zaidi kuhusu jinsi ya kutumia zana hizi zinapatikana kwenye tovuti ya shirika la Rainforest Alliance: Mpango wa Uidhinishaji. Mahitaji ya ziada kuhusu poligoni za vitengo vya shamba: - Poligoni za vipande vya mashamba hazipaswi kuingiliana zaidi ya 20% ya eneo lake na poligoni nyingine. - Poligoni za vitengo vya mashamba zinapaswa kuwa na jiometri sahihi. - Poligoni za vitengo vya mashamba vilivyo karibu zinaweza kushiriki mpaka wa pamoja. - Mipaka inayofuata vipengele vinavyoonekana kwa urahisi kwenye picha (kama vile barabara na mito) inaweza kutumika kuboresha usahihi wa uchoraji wa poligoni. ### 1.5 Kuripoti Data Jedwali lililo hapa chini linaonyesha aina na miundo ya faili inayohitajika kwa ajili ya kuripoti data za eneo la kijiografia kwenye jukwaa la shirika la Rainforest Alliance. **Jedwali 1.** Miundo na violezo vinavyokubalika vya data za eneo la kijiographia | **Mahitaji ya viwango** | **Kuwasilishwa** | **Aina ya faili inayokubalika** | | --- | --- | --- | | **1.2.10** (100% ya data za eneo la kijiografia za vitengo vya mashamba vyenye mazao yaliyoidhinishwa) | **Faili moja** yenye alama za eneo. | Kichupo “3. Kitengo cha Shamba” cha kiolezo cha Sajili ya Wanachama wa Kundi (GMR) (kwa kutumia safu wima za latitudo na longitudo). | | **Faili moja** yenye poligoni. | KML au GeoJSON. | | **1.2.11** | **Faili moja** yenye poligoni za shamba, ikijumuisha vitengo vyote vya mashamba. | KML au GeoJSON. | #### 1.5.1 Mambo mengine ya kuzingatia katika kuripoti data: 1. Wakati mashamba makubwa ni sehemu ya kikundi, hitaji 1.2.11 linatumika kwa mashamba hayo makubwa. Faili ya data za eneo la kijiografia iliyowasilishwa inapaswa kuwa na poligoni za mashamba yote makubwa ambayo ni sehemu ya kikundi. 2. Wakati wa kujiandaa kwa ukaguzi wa kwanza, Mmiliki wa Cheti lazima apakie faili za data za eneo la kijiografia zilizotajwa katika jedwali la 2 hapo juu kwenye jukwaa la uidhinishaji la shirika la Rainforest Alliance. 3. Mumiliki wa Cheti anaweza kuwasilisha faili za ziada za poligoni tu baada ya kuwa tayari amewasilisha Rejesta ya Wanachama wa Kundi lililoidhinishwa kwenye jukwaa la shirika la Rainforest Alliance. 4. Wakati wa kutoa alama za eneo, data zifuatazo lazima zitolewe kupitia kichupo cha 3 cha Rejesta ya Wanachama wa Kundi kwa kila kitengo cha shamba: - Kitambulisho cha Kipekee cha Ndani cha Shamba (ili kutambua shamba kama sehemu ya kundi). - Kitambulisho cha kitengo cha shamba (ili kuunganisha kitengo cha shamba na shamba ambalo ni sehemu yake). - Eneo la kitengo cha shamba (hekta). - Viwianishi vya latitudo (muundo wa DD). - Viwianishi vya longitudo (muundo wa DD). 5. Wakati wa kuwasilisha faili za poligoni, yafuatayo lazima yahakikishwe kwa kila kitengo cha shamba: - Poligoni zinaambatanishwa na kitambulisho cha kipekee cha kitengo cha shamba. - Kabla ya kupakia poligoni, kitengo cha shamba lazima kiwe tayari kimesajiliwa katika sehemu ya taarifa za mashamba kwenye jukwaa la shirika la Rainforest Alliance. (Kwa uidhinishaji wa kikundi, taarifa za shamba hujazwa kiotomatiki kulingana na taarifa zilizotolewa katika Rejesta ya Wanachama wa Kundi). ## 2. Ukaguzi wa ndani ### 2.1 Wigo wa Ukaguzi wa Ndani Hitaji la msingi 1.4.1 la Viwango vya shirika la Rainforest Alliance linahitaji usimamizi kuanzisha mfumo wa ukaguzi wa ndani ili kuhakikisha utekelezaji wa mahitaji ya Viwango vya shirika la Rainforest Alliance miongoni mwa wanachama wote wa kundi. Usimamizi lazima utoe rasilimali zote zinazohitajika ili kuhakikisha utendakazi mzuri wa mfumo wa ukaguzi wa ndani. Usimamizi wa Wamiliki wa Vyeti wanaoingia katika mpango wa uidhinishaji lazima uhakikishe kuwa wahusika wote walio katika wigo wa uidhinishaji wanakaguliwa ndani kwa kuzingatia mahitaji yote yanayotumika ya kiwango kabla ya ukaguzi wa kwanza wa uidhinishaji. Kwa ukaguzi unaofuata, ukaguzi wa ndani unategemea kiwango cha hatari pamoja na matokeo ya ukaguzi uliotangulia na ukaguzi wa nje. Zaidi ya hayo, wigo wa ukaguzi wa ndani unaofuata umeainishwa katika jedwali hapa chini: **Jedwali 2.** Upeo wa ukaguzi wa ndani kwa kulingana na aina na muundo wa shamba. | **Aina ya shamba** | **Wigo wa ukaguzi wa ndani** | | --- | --- | | Shamba kubwa | Mashamba yote yanapaswa kukaguliwa kila mwaka. - Vitengo vyote vya mashamba vinapaswa kukaguliwa. | | Mashamba madogo | Angalau 35% ya mashamba yanapaswa kukaguliwa kila mwaka, huku ikihakikisha kuwa mashamba yote yanakaguliwa baada ya miaka mitatu mfululizo. **Kumbuka:** Shirika la Rainforest Alliance linahifadhi haki ya kuhitaji sampuli kubwa kwa zao fulani au katika nchi au eneo mahususi. | | Mashamba madogo yenye vi vitengo vingi vya mashamba | Uteuzi wa vitengo vya mashamba vitakavyokaguliwa unategemea: - Hatari (kwa mfano, ukaribu na misitu, mifumo mingine ya asili ya ikolojia, vyanzo vya maji, n.k.) - Iwapo kitengo cha shamba kimewahi kutembelewa hapo awali au la. | > [!WARNING] > **Kumbuka:** wanachama wote wapya wanahitaji kukaguliwa kikamilifu kwa kuzingatia mahitaji yote ya kiwango yanayotumika, kabla ya ukaguzi wa nje. ### 2.2 Mafunzo ya Wakaguzi wa Ndani Usimamizi lazima uhakikishe kuwa wakaguzi wa ndani wamepata mafunzo ya kutosha ili kufanya ukaguzi wa ndani wenye ubora. Mafunzo hayo yanapaswa kutolewa na wataalamu wenye uwezo na ujuzi wa kitaalamu kuhusu utekelezaji na ukaguzi wa Viwango vya shirika la Rainforest Alliance. Usimamizi lazima pia uhakikishe kuwa wakaguzi wote wa ndani wamekamilisha kozi zote zinazohitajika kwenye Mtandao wa Mafunzo wa shirika la Rainforest Alliance na kukamilisha tathmini zinazohitajika. Zaidi ya hayo, uongozi unahitajika kutoa mafunzo ya kila mwaka kwa wakaguzi wote, kuhusu mbinu sahihi za ukaguzi wa ndani, yakiwemo tathmini za kila mwaka kulingana na hitaji la 1.3.3. ## 3. Ufafanuzi wa matumizi ya mahitaji ya msingi 1.1.1 na 1.4.3 Wamiliki wa Vyeti walioidhinishwa au wanaotafuta uidhinishaji chini ya Kiwango cha Kilimo Rejelevu lazima wazingatie mahitaji ya msingi 1.1.1 na 1.4.3. Aidha, mahitaji ya Msingi yanayorejelea Kiwango cha Kilimo Endelevu cha shirika la Rainforest Alliance yatachukuliwa kuwa yanarejelea Kiwango cha Kilimo Rejelevu cha shirika la Rainforest Alliance. ## Taarifa nyinginezo Tarehe ya kwanza ya kuchapishwa kwa hati hii (v 1.0): Julai 1, 2022. Nyaraka zilizotajwa kuwa *"zinazofunganisha"* lazima zizingatiwe ili kupata uthibitisho. Nyaraka zinazotajwa kama *"zisizo funganisha"* hutoa taarifa zisizo za lazima ili kuwasaidia wasomaji kuelewa na kutekeleza masharti pamoja na maudhui mengine yanayolazimisha. **Kanusho la Tafsiri** Kwa swali lolote linalohusiana na maana kamili ya taarifa katika tafsiri, rejelea toleo rasmi la Kiingereza kwa ufafanuzi. Makosa yoyote au tofauti za maana zinazotokana na tafsiri, hazilazishi na hazina athari kwa madhumuni ya ukaguzi au uthibitisho. Unakili, urekebishaji, usambazaji, au uchapishaji upya wa maudhui haya ni marufuku kabisa bila idhini ya maandishi ya awali kutoka kwa shirika la Rainforest Alliance. **Taarifa zaidi?** Kwa msaada wa kupata cheti cha shirika la Rainforest Alliance, wasiliana na timu yetu ya Huduma kwa Wateja kupitia [customersuccess@ra.org](mailto:customersuccess@ra.org). Kwa taarifa zaidi kuhusu shirika la Rainforest Alliance, tembelea [http://www.rainforest-alliance.org](http://www.rainforest-alliance.org) wasiliana kupitia [info@ra.org](mailto:info@ra.org) au Ofisi ya shirika la Rainforest Alliance Amsterdam, De Ruijterkade 6, 1013AA Amsterdam, Uholanzi.