--- title: "Kiambatisho cha Kijamii v1.3" slug: "social-annex-v13-swahili" status: "new" updated: 2026-11-20T09:38:35Z published: 2026-11-20T09:38:35Z canonical: "knowledge.rainforest-alliance.org/social-annex-v13-swahili" --- > ## Documentation Index > Fetch the complete documentation index at: https://knowledge.rainforest-alliance.org/llms.txt > Use this file to discover all available pages before exploring further. # Kiambatisho cha Kijamii v1.3 ![](https://cdn.document360.io/929f3fed-0f9d-454a-80e4-d7496bf45e88/Images/Documentation/indicator-guidance-image-g96v93xw.png?sv=2026-02-06&spr=https&st=2026-11-20T20%3A55%3A21Z&se=2026-11-20T21%3A55%3A21Z&sr=b&sp=r&sig=p0fpJc5wPJXU%2F5k6XDwZVZM8bWSo4qMpzhA4r2gIkRs%3D) | Kichwa: | Kiambatisho cha Kijamii | | --- | --- | | Msimbo: | A-08-SCRL-B-CH | | Toleo: | 1.3 | | Inatumika kwa: | Wamiliki wa Vyeti vya Kilimo na Mnyororo wa Ugavi | | Utekelezaji: | Maudhui ya kuunganisha | | Kuanzia: | Machi 1, 2026 | | Inakamilika ifikapo: | Hadi itakapotangazwa vinginevyo | | Imechapishwa mnamo: | Septemba 8, 2025 | | Imeunganishwa na: | [A-1-S-B-F-V1.4 Kiwango cha Kilimo Endelevu cha shirika la Rainforest Alliance.](https://knowledge.rainforest-alliance.org/docs/rainforest-alliance-sustainable-agriculture-standard-farm-requirements-swahili) [A-33-R-B-FA-V1.0 Kiwango cha Kilimo Rejelevu cha shirika la Rainforest Alliance.](https://knowledge.rainforest-alliance.org/docs/rainforest-alliance-regenerative-agriculture-standard-swahili) [A-35-SRCL-B-SC_V1.5 Mahitaji ya Mnyororo wa Ugavi wa shirika la Rainforest Alliance.](https://knowledge.rainforest-alliance.org/docs/rainforest-alliance-supply-chain-requirements-v15) | | Inachukua nafasi ya: | [A-08-SCRL-B-CH-V1.2- Kiambatisho cha Kijamii.](https://knowledge.rainforest-alliance.org/docs/social-annex) | ### Hati hii inahusu nini? Kiambatisho hiki kinajumuisha maudhui ya ziada yenye masharti ya lazima kuhusu matakwa yaliyo katika Sura ya Kijamii ya Viwango vya shirika la Rainforest Alliance na Mahitaji ya Mnyororo wa Ugavi ya shirika la Rainforest Alliance. Hati hii inajumuisha: - Muhtasari wa Itifaki ya shirika la Rainforest Alliance ya Kushughulikia na Kurekebisha Ukiukaji wa Mahitaji. - Muhtasari wa mchakato wa Ridhaa Huru, ya Awali na Yenye Taarifa Kamili (FPIC). - Taarifa za ramani za Hatari za Ajira ya Watoto na Ajira ya Kulazimishwa kwa ajili ya Kiwango cha Kilimo Endelevu. - Taarifa kuhusu viwango vya Mshahara unaokidhi mahitaji ya msingi ya maisha kwa kila nchi, kwa ajili ya Kiwango cha Kilimo Endelevu. ### Lini na jinsi ya kutumia hati hii? Hati hii inawapa Wamiliki wa Vyeti na Mashirika ya Uidhinishaji maelezo ya ziada kuhusu mahitaji yaliyomo na jinsi ya kuyatekeleza. Hati hii imegawanywa katika sehemu tatu: - Mahitaji ya msingi kutoka viwango vya Mashamba na Mahitaji ya Mnyororo wa Ugavi - Mahitaji ya Msingi kutoka viwango vya Mashamba. - Mahitaji kutoka Kiwango cha Kilimo Endelevu pekee Sehemu ya kwanza ina mahitaji yanayotumika kwa viwango vyote vya Mashamba na Mahitaji ya Mnyororo wa Ugavi. Mahitaji ya msingi yanatumika kwa viwango vyote vya Mashamba. Mahitaji katika sehemu ya Kiwango cha Kilimo Endelevu yanajumuisha mahitaji maalum na mahitaji ya uboreshaji endelevu yanayotumika kwa kiwango hiki. ## Mabadiliko katika toleo lililosasishwa kutoka v1.1 hadi v1.2 | **Sehemu** | **Nini kimebadilika** | | --- | --- | | Katika hati nzima | Ongezo la Kiwango cha Kilimo Rejelevu cha shirika la Rainforest Alliance. | | Katika hati nzima | Kujumuishwa kwa sehemu mbili kuu: ya kwanza inahusu mahitaji ya msingi ya viwango vya Mashamba na mahitaji ya Mnyororo wa Ugavi, na ya pili inahusu mahitaji ya Kiwango cha Kilimo Rejelevu pekee. | ## Mahitaji ya msingi kutoka viwango vya Mashamba na Mahitaji ya Mnyororo wa Ugavi Sehemu hii inatoa maelezo zaidi kuhusu utekelezaji wa mahitaji husika ya msingi ya Kiwango cha Kilimo Endelevu cha shirika la Rainforest Alliance (SAS), Kiwango cha Kilimo Rejelevu (RAS), na Mahitaji ya Mnyororo wa Ugavi ya shirika la Rainforest Alliance. ## 1. Itifaki ya shirika la Rainforest Alliance ya Kushughulikia na Kurekebisha Ukiukaji wa Mahitaji **Inahusiana na mahitaji ya msingi 1.5.1, 1.6.2, 5.1.4 na mahitaji ya Mnyororo wa Ugavi 1.4.1 na 4.1.4** Sehemu hii inaelezea Itifaki ya shirika la Rainforest Alliance ya Kushughulikia na Kurekebisha Ukiukaji wa Mahitaji, na kubainisha hatua za lazima ambazo Wamiliki wote wa Vyeti wanapaswa kufuata ili kushughulikia ipasavyo visa vya ajira ya watoto, ajira ya kulazimishwa, ubaguzi, ukatili na unyanyasaji mahali pa kazi. Uongozi wa Mmiliki wa Cheti lazima uhakikishe kuwa Itifaki ya Kushughulikia na Kurekebisha Ukiukaji wa Mahitaji inaanza kutekelezwa mara moja baada ya kisa kutambuliwa, kuchunguzwa na kuthibitishwa. Hatua za ziada za hiari na mwongozo kuhusu jinsi ya kutekeleza shughuli za kurekebisha ukiukaji wa mahitaji kwa mujibu wa Itifaki hii zinapatikana katika Mwongozo S wa shirika la Rainforest Alliance: Itifaki ya Kushughulikia na Kurekebisha Ukiukaji wa Mahitaji. ### 1.1 Kuanzisha Mfumo wa Kushughulikia na Kurekebisha Ukiukaji wa Mahitaji Hatua zifuatazo ni za kujiandaa kwa ajili ya kurekebisha ukiukaji wa mahitaji kwa ufanisi, kwa kuanzisha kwanza mfumo wa urekebishaji. #### 1.1.1 Kuteua wahusika wanaowajibika Kwa Wamiliki wa Vyeti cha Mashamba, uongozi huteua kamati moja au kadhaa zinazowajibika kusimamia Utaratibu wa Kushughulikia malalamiko, mfumo wa Tathmini na Ushughulikiaji, na usawa wa jinsia. Kwa uthibitishaji wa kikundi, badala ya kuunda kamati, anaweza kuteuliwa mtu anayewajibika, anayewakilisha uongozi na mwenye mamlaka ya kufanya maamuzi ili kusimamia mfumo wa Tathmini na Ushughulikiaji na masuala ya usawa wa kijinsia. Kwa Wamiliki wa Vyeti vya Mnyororo wa Ugavi, uongozi huteua kamati moja au kadhaa zinazowajibika kusimamia Utaratibu wa Kushughulikia Malalamiko na Mfumo wa Tathmini na Ushughulikiaji. #### 1.1.2 Maandalizi ya Mpango wa Kurekebisha Ukiukaji wa Mahitaji Shirika la Rainforest Alliance linawataka Wamiliki wa Vyeti kujumuisha Mpango wa Kurekebisha Ukiukaji wa Mahitaji katika mpango wao wa usimamizi. Hii huhakikisha kuwa hatua za kushughulikia visa zinachukuliwa haraka mara vinapotambuliwa. Hatua za kuandaa mpango wa kurekebisha ukiukaji wa mahitaji zimeainishwa hapa chini. **i. Tambua na Uorodheshe Wadau** Kamati au mtu anayewajibikia mfumo wa Tathmini na Ushughulikiaji lazima atambue wadau wa ndani na nje wanaoweza kushiriki katika kurekebisha ukiukaji wa mahitaji, kama vile viongozi wa jamii, mashirika ya wanawake, vilabu vya vijana, taasisi za serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na mashirika ya haki za binadamu. Tazama Mwongozo S wa shirika la Rainforest Alliance: Itifaki ya Kushughulikia na Kurekebisha Ukiukaji wa Mahitaji, kwa mfano wa jinsi ya kutambua na kuorodhesha wadau wa nje wanaohusika. **ii. Tengeneza Mpango wa Kurekebisha Ukiukaji wa Mahitaji** Mpango wa Kurekebisha Ukiukaji wa Mahitaji huandaliwa na kamati ya Tathmini ya Ushughulikiaji au mtu anayewajibika, kwa msaada wa Kamati ya Jinsia au mtu anayewajibikia Wamiliki wa Vyeti vya Mashamba. Kwa Wamiliki wa vyeti vya Mnyororo wa Ugavi, mpango huo huandaliwa na Kamati ya Tathmini na Ushughulikiaji au mwakilishi wa usimamizi. Mpango huu unaainisha hatua zinazopaswa kutekelezwa ili kurekebisha kisa kilichothibitishwa na kutambua wadau watakaohusika katika mchakato huo. Kwa kila hatua, mpango lazima ubainishe wazi mahali na wakati itakapotekelezwa, tarehe ya kuanza na ya kukamilika, pamoja na watu watakaowajibika katika utekelezaji wake. Utekelezaji wa mpango lazima ufuatiliwe, na maendeleo yaliyopatikana lazima yaandikwe na kuhifadhiwa kama kumbukumbu. Tazama Mwongozo S wa shirika la Rainforest Alliance: Itifaki ya Kushughulikia na Kurekebisha Ukiukaji wa Mahitaji ili kupata kiolezo cha mfano cha Mpango wa Kurekebisha Ukiukaji wa Mahitaji. **iii. Mafunzo na Uhamasishaji** Baada ya kuandaliwa kwa mpango wa kurekebisha ukiukaji wa mahitaji, wajumbe wa kamati, akiwemo mwakilishi wa usimamizi, watapokea mafunzo kuhusu majukumu yao husika pindi kisa kinachoweza kuashiria ukiukaji kinapogunduliwa na kuripotiwa. Wanachama wa kikundi/wafanyakazi au waajiriwa watafahamishwa kuhusu Mfumo wa kushughulikia malalamiko na Itifaki ya Kushughulikia na kurekebisha ukiukaji wa mahitaji; haki zao na jinsi wanavyoweza kupata huduma za kurekebishiwa madhara yaliyotokana na ukiukaji huo. #### 1.2 Kisa Kinapotokea: Mchakato wa Kukabiliana na Kisa na Kurekebisha ukiukaji wa mahitaji Jedwali lililo hapa chini linaainisha hatua zinazohitajika za kushughulikia malalamiko na kurekebisha ukiukaji wa mahitaji, hatua za mchakato, muda wa kutekeleza kila hatua na wahusika wanaowajibika katika kukabiliana na visa vya ajira ya watoto, ajira ya kulazimishwa, ubaguzi, ukatili na unyanyasaji mahali pa kazi. Katika baadhi ya visa, shirika la Rainforest Alliance linaweza kuidhinisha mabadiliko ya muda uliowekwa, iwapo sababu za kufanya hivyo zimeelezwa na kuhalalishwa ipasavyo. Hatua za ziada za hiari na mwongozo kuhusu jinsi ya kutekeleza hatua za lazima, zinapatikana katika Mwongozo wa S wa shirika la Rainforest Alliance: Itifaki ya Kushughulikia na Kurekebisha Ukiukaji wa Mahitaji. | **Muda wa utekelezaji kwa wiki**[**[1]**](/docs/social-annex-v13-swahili#footnote-2) | **Hatua** | **Shughuli** | **Mhusika anayewajibika** | | --- | --- | --- | --- | | saa 48 | **1. Kisa kimeripotiwa** | Kesi kinapopokelewa/kutambuliwa na kamati au mifumo yoyote, kinawasilishwa kwa Kamati ya Kushughulikia Malalamiko (GC) na Kamati ya Jinsia[[2]](/docs/social-annex-v13-swahili#footnote-3) kwa ajili ya uchunguzi na uthibitishaji wa kisa hicho. | Kamati ya Kushughulikia Malalamiko, Kamati ya Tathmini na Ushughulikiaji (A&A) / Kamati ya Usawa wa Kijinsia | | saa 48 | **2. Majibu** Hatua za haraka za kulinda usalama na ustawi waathiriwa | Mara tu kisa kinaporipotiwa, usalama na ulinzi wa mtu aliye katika hatari lazima vipewe kipaumbele. Msaada hutolewa pale ambapo kuna hatari ya haraka ya madhara kwa afya ya akili au ya mwili ya wafanyakazi katika kisa kinachotambuliwa au kuripotiwa. Iwapo msaada wa wataalamu wa nje unahitajika, ni lazima utolewe tu baada ya kupata ridhaa kamili ya mhusika na kuhakikisha usiri wa taarifa zake. | Usimamizi wa Mmiliki wa Cheti, Kamati ya Kushughulikia Malalamiko, Kamati ya Tathmini na Ushughulikiaji / Kamati ya Usawa wa Kijinsia | | wiki 4 | **3. Majibu** tathmini ya kiwango cha uzito wa kisa | Kamati ya Kushughulikia Malalamiko (GC) hufanya tathmini ya kiwango cha uzito wa kisa kwa msaada wa kamati ya Tathmini na Ushughulikiaji (A&A) au Kamati ya Usawa wa Kijinsia, kwa kutumia maswali hapa chini. Ikiwa jibu lolote ni 'Ndiyo', kisa hicho kinachukuliwa kuwa cha uzito wa juu. Uchunguzi zaidi lazima uendelee kwa kufuata hatua zilizoainishwa hapa chini. Huenda mamlaka za mitaa zikahitajika kuhusishwa kwa ridhaa ya mlalamikaji. Ikiwa majibu yote ni 'Hapana', kisa hicho hakichukuliwi kuwa na uzito wa juu. Kamati ya Kushughulikia Malalamiko (GC) huhitimisha uchunguzi na kuamua hatua za kurekebisha ukiukaji wa mahitaji. | Kamati ya Kushughulikia Malalamiko, Kamati ya Tathmini na Ushughulikiaji (A&A) / Kamati ya Usawa wa Kijinsia | | **Maswali ya Kutathmini Kiwango cha Uzito wa Kisa** 1. Je, hali ya mwajiriwa/mfanyakazi/mtoto/mtu au watu wanaoweza kutoa taarifa kuhusu ukiukaji wa masharti, inahatarisha maisha yake? 2. Je, hili ni tukio la kimfumo, yaani, kuna visa vingi vya hili katika shamba au eneo la kazi? 3. Je, hali hii inaweza kusababisha madhara ya kudumu kwa ustawi wa mwajiriwa/mfanyakazi au mtoto, yakiwemo madhara ya kimwili na/au kisaikolojia? 4. Je, kuna ushahidi kwamba usimamizi au mfanyakazi alikuwa anafahamu kuwa ukiukaji huo ulikuwa ukiendelea, lakini akaendeleza na/au akaidhinisha kitendo hicho? | | wiki 12[[3]](/docs/social-annex-v13-swahili#footnote-4) | **4. Urekebishaji:** Tekeleza marekebisho na uandae mpango wa hatua za kuzuia marudio ya ukiukaji | Urekebishaji unatekelezwa kulingana na Mpango wa Urekebishaji. Usimamizi wa Mmiliki wa Cheti (kwa kushirikiana na wahusika wa nje) hutekeleza marekebisho yaliyokubaliwa na Kamati ya Kushughulikia Malalamiko (GC), kamati ya Tathmini na Ushughulikiaji (A&A) na/au kamati ya usawa wa Kijinsia. Mpango wa hatua za kurekebisha na kuzuia kujirudia kwa ukiukaji huandaliwa ukiwa na ratiba ya kina ya utekelezaji. Mpango huo lazima ujumuishe kila mara hatua za kuhakikisha kuwa ukiukaji hautokei tena, kwa kuzingatia uchambuzi wa chanzo kikuu cha ukiukaji huo, kwa msaada wa Kamati ya Tathmini na Ushughulikiaji (A&A) na/au Kamati ya Usawa wa Kijinsia. | Usimamizi wa Mmiliki wa Cheti, Kamati ya Tathmini na Ushughulikiaji (A&A)/Kamati ya Usawa wa Kijinsia | | wiki 52[[4]](/docs/social-annex-v13-swahili#footnote-5) | **5. Urekebishaji** tekeleza mpango wa hatua za kurekebisha | Usimamizi wa Mmiliki wa Cheti (pamoja na wahusika wa nje) hutekeleza hatua za kurekebisha ili kushughulikia chanzo kikuu cha tatizo kwa msaada wa kamati. | Usimamizi wa Mmiliki wa Cheti, Kamati ya Tathmini na Ushughulikiaji / Kamati ya Jinsia | | Katika hati nzima | **6. Urekebishaji** – ufuatiliaji | Kamati ya Tathmini na Ushughulikiaji (A&A)/Kamati ya Usawa wa Kijinsia hufuatilia utekelezaji wa marekebisho yaliyokubaliwa na hatua za kurekebisha ukiukaji zinazotekelezwa na usimamizi wa Mmiliki wa Cheti (CH) na wadau wa nje. | Kamati ya Tathmini na Ushughulikiaji / Kamati ya Jinsia | ## Mahitaji ya msingi kwa viwango vya Shamba Sehemu hii inatoa maelezo ya ziada kuhusu utekelezaji wa mahitaji husika ya msingi ya Kiwango cha Kilimo Endelevu cha shirika la Rainforest Alliance (SAS) na Kiwango cha Kilimo Rejelevu (RAS). ## 2. Mchakato wa Ridhaa Huru, ya Awali na yenye Taarifa Kamili (FPIC) **Inahusiana na mahitaji ya msingi 5.8.1 na 5.8.2** Hitaji la 5.8.1 la viwango vya shirika la Rainforest Alliance linaeleza kuwa usimamizi wa mashamba makubwa na ya kibinafsi yaliyoidhinishwa lazima uheshimu haki za kisheria na za kimila za watu wa jamii za asili na jamii za wenyeji. Shughuli zinazoathiri haki za matumizi ya ardhi au rasilimali, au maslahi ya pamoja ya watu wa jamii za asili na jamii za wenyeji, ikiwemo maeneo yenye Thamani za Juu za Uhifadhi (HCV) 5 na 6, hufanyika tu baada ya kupata ridhaa huru, ya awali na yenye taarifa kamili (FPIC). Kwa mujibu wa sharti la 5.8.2, iwapo watu wa jamii za asili na/au jamii za wenyeji wanapinga haki za matumizi ya ardhi za mzalishaji, mashamba makubwa na mashamba yaliyoidhinishwa kibinafsi lazima yafuate mchakato wa FPIC, kama sehemu ya hatua za kuthibitisha kuwa yana haki halali ya kutumia ardhi hiyo. Sehemu hii ina hatua za lazima za kufuata katika mchakato wa FPIC. Mwongozo na mifano ya jinsi ya kutekeleza mchakato wa FPIC inapatikana katika Mwongozo T wa shirika la Rainforest Alliance: Michakato ya Ridhaa ya Hiari, ya Awali na Yenye Taarifa Kamili (FPIC) ### 2.1 Utumikaji: #### 2.1.1 Miradi au Shughuli Zinazohitaji Mchakato wa FPIC Michakato ya Ridhaa ya Hiari, ya Awali na Yenye Taarifa Kamili FPIC inahitajika ikiwa shughuli zozote kati ya zifuatazo zinapendekezwa na zinaweza kuwa na athari hasi kwa haki, ardhi, rasilimali, maeneo, riziki, au utoshelevu wa chakula wa watu wa jamii za asili au jamii za wenyeji. Michakato ya FPIC inahitajika ikiwa mradi au shughuli itahusisha: 1. Kubadilisha ardhi isiyotumika kwa kilimo kuwa ardhi ya uzalishaji wa mazao. 2. Kubadilisha ardhi ya kilimo ya wakulima wadogo, ambayo hutumika hasa kwa kilimo cha kujikimu au kwa matumizi ya wenyeji, kuwa ardhi ya kulima mazao kwa ajili ya biashara na matumizi nje ya eneo husika. 3. Kubadilisha maeneo ya jadi ya malisho kuwa matumizi mengine ya ardhi ya kilimo ambayo yanazuia au kupunguza shughuli za awali za malisho. 4. Kuongeza kiwango cha uchotaji wa maji katika eneo fulani kwa kiwango kinachoweza kupunguza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa maji kwa watumiaji wengine wa karibu au wa maeneo ya chini ya mkondo wa maji. 5. Kusitisha au kupunguza ufikiaji wa jamii za wenyeji kwenye mifumo ya ikolojia ya asili au maeneo mengine ambayo kwa sasa hutumika kwa uwindaji, uvuvi, au ukusanyaji wa mimea au sehemu zake kwa ajili ya chakula, nyuzi, nishati, dawa, au bidhaa nyingine. 6. Kufanyika ndani au karibu na maeneo yanayotumiwa na watu wa jamii za wenyeji kwa shughuli za jadi za kitamaduni au kidini, au maeneo yaliyoainishwa kuwa na Thamani ya Juu ya Uhifadhi (HCV) kwa mujibu wa ufafanuzi ufuatao: HCV5: Maeneo na rasilimali muhimu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya msingi ya jamii za wenyeji au watu wa jamii za asili (kama vile riziki, afya, lishe, maji, n.k.), yaliyotambuliwa kwa kushirikiana na jamii hizo au watu wa jamii za asili. HCV6: Maeneo, rasilimali, makazi ya viumbe na mandhari yenye umuhimu wa kitamaduni, kiakiolojia au kihistoria duniani au kitaifa, pamoja na yale yenye umuhimu mkubwa wa kitamaduni, kiikolojia, kiuchumi, au kidini/kitakatifu kwa tamaduni za jadi za jamii za wenyeji au watu wa jamii za asili. Haya hutambuliwa kupitia mashauriano na jamii hizo za wenyeji au watu wa jamii za asili. Hatua zilizoainishwa hapa chini zinaelezea jinsi mchakato wa FPIC unapaswa kutekelezwa. Hatua ya 1 (kubainisha wigo) inahitajika katika michakato yote ya FPIC. Kwa kuzingatia matokeo ya Hatua ya 1: 1. Ikiwa miradi au shughuli zilizopendekezwa hazipunguzi haki za watu wa jamii za asili na jamii za wenyeji, mwombaji huchukuliwa kuwa ametimiza sharti la 5.8.1. 2. Ikiwa miradi au shughuli zilizopendekezwa zinapunguza haki za matumizi ya ardhi au rasilimali au maslahi ya pamoja ya watu wa jamii za asili au jamii za wenyeji (ikiwemo maeneo yenye Thamani ya Juu ya Uhifadhi (HCV) 5 au 6), mwombaji huchukuliwa kuwa ametimiza sharti hilo tu ikiwa hatua za 2 - 6 za Sehemu ya 4.2 (Utekelezaji wa Mchakato wa FPIC) zimetekelezwa. #### 2.1.2 Shughuli za Uendeshaji Zisizohitaji Mchakato wa FPIC Shughuli zilizoidhinishwa zilizokuwa na cheti halali cha shirika la Rainforest Alliance kufikia Juni 1, 2020, na ambazo hazipangi kuanzisha miradi au shughuli zozote zinazohitaji mchakato wa FPIC (kama ilivyofafanuliwa katika sehemu iliyo hapo juu), wala kupanua wigo wa shughuli baada ya Juni 1, 2020, huchukuliwa kuwa zimetimiza sharti la 5.8.1 kwa sababu zilikuwa zimetimiza kigezo cha msingi cha 4.20 cha Kiwango cha Kilimo Endelevu cha shirika la Rainforest Alliance cha mwaka 2017. Hitaji la 5.8.1 halitumiki kwa shughuli zinazohitaji uidhinishaji kwa mara ya kwanza kuanzia Juni 1, 2020 na kuendelea, ambazo hazipangi kuanzisha miradi au shughuli zozote zinazohitaji mchakato wa FPIC (kama ilivyofafanuliwa katika sehemu iliyo hapo juu). ### 2.2 Utekelezaji wa Mchakato wa FPIC Mchakato wa Ridhaa Huru, ya Awali na yenye Taarifa Kamili (FPIC) lazima ufuate hatua sita zilizofupishwa hapa chini. **Mchoro 1.** Hatua za Mchakato wa Ridhaa Huru, ya Awali na yenye Taarifa (FPIC) ![](https://cdn.document360.io/929f3fed-0f9d-454a-80e4-d7496bf45e88/Images/Documentation/Swahili TOC Graphic.png?sv=2026-02-06&spr=https&st=2026-11-20T20%3A55%3A21Z&se=2026-11-20T21%3A55%3A21Z&sr=b&sp=r&sig=59iNGPBMyN5KYcmn7WPzOKJKpnk%2BARfz3SueiUrm43w%3D) #### Hatua ya 1 – Kubainisha wigo 1. Tambua watu wa jamii za asili na jamii za wenyeji ambao huenda wananufaika na ardhi au rasilimali ambazo shamba linapendekeza kuendeleza, kumiliki, kutumia, au kunufaika nazo, au ambao wanaweza kuathiriwa na shughuli, mradi, au upanuzi uliopendekezwa. 2. Tambua haki, madai, au maslahi ya jamii hizi kuhusiana na ardhi au rasilimali (k.m., haki za maji, maeneo ya kupata maji, au haki za kuwinda au kukusanya mazao ya misitu) ndani au karibu na eneo/maeneo ya shughuli, mradi, au upanuzi uliopendekezwa. 3. Bainisha maeneo, rasilimali, makazi ya viumbe na mandhari yoyote yenye umuhimu wa kitamaduni, kiakiolojia, kihistoria duniani au kitaifa, au yenye umuhimu mkubwa kwa tamaduni za jadi za jamii za wenyeji au watu wa asili, ambayo yanaweza kuathiriwa na shughuli, mradi au upanuzi unaopendekezwa. Utambuzi huu unapaswa kufanywa kupitia mashauriano na jamii hizi za wenyeji au watu wa asili. 4. Bainisha ikiwa shughuli, mradi, au upanuzi uliopendekezwa unaweza kupunguza haki, madai, au maslahi yaliyotambuliwa katika Hatua ya 1 – b na c. Hali hii hutokea katika mazingira yanayojumuisha, lakini yasiyopungukia yafuatayo: 1. Ardhi inayotumiwa kwa sasa na jamii au wanajamii kwa shughuli kuu za kujikimu kimaisha. 2. Jamii au wanajamii watakosa kabisa au watapunguziwa fursa ya kupata rasilimali za asili zinazotumika kwa matumizi ya ndani au kujikimu kimaisha. #### Hatua ya 2 – Upangaji, utafiti, na tathmini 1. Fanya uchoraji wa ramani shirikishi wa matumizi ya ardhi na rasilimali za asili. 2. Tathmini athari zinazoweza kusababishwa (chanya na hasi) na mradi. 3. Shirikisha wahusika huru kusaidia mchakato wa uchoraji ramani na tathmini. Jamii zina haki ya kuchagua mhusika huru wa kuzisaidia katika mchakato wa Ridhaa Huru, ya Awali na Inayofahamishwa (FPIC). Wahusika hawa huru wanaweza kujumuisha mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ya ndani. Wahusika huru wanapaswa pia kushirikishwa katika mchakato wa FPIC ili kuthibitisha bila upendeleo uzingatiaji wa hatua na makubaliano ya mchakato huu. 4. Fafanua upya na kurekebisha mradi, inapohitajika, ili kushughulikia athari zinazoweza kujitokeza kuhusiana na haki za watu wa asili na jamii za wenyeji. #### Hatua ya 3 – Mashauriano 1. Wape wawakilishi wa jamii maelezo kuhusu shughuli za mradi, manufaa na athari zake, kwa namna inayoeleweka na inayozingatia viwango vya elimu vya wawakilishi hao pamoja na muktadha wa kitamaduni wa jamii husika. 2. Toa muda wa kufanya mashauriano ya ndani kwa ndani ili kujadili na kuamua kama mradi unaopendekezwa unakubalika. 3. Shauriana na jamii ili kubaini kama inakubali mradi (uamuzi wa KUENDELEA / KUSITISHA), na masharti ambayo jamii inaweka kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. 4. Fafanua upya na kurekebisha mradi, inapohitajika, ili kushughulikia hoja na wasiwasi ulioibuliwa na jamii wakati wa mashauriano. #### Hatua ya 4 – Majadiliano 1. Iwapo jamii itakubali mradi, jadiliana kuhusu masharti ya makubaliano ya utekelezaji wa mradi. Masharti haya yanapaswa kujumuisha kuendelea kupata na kutumia ardhi na rasilimali zilizoathiriwa, fidia ya haki na inayolingana na kiwango cha upotevu wa matumizi ya ardhi na rasilimali, na/au mgao wa haki wa manufaa yanayotokana na mradi. 2. Wezesha jamii kupata ushauri wa kisheria ili kuzisaidia katika mchakato wa majadiliano, inapohitajika. Ushauri wa kisheria na upatikanaji wa wahusika huru vinapaswa kupatikana kwa jamii katika kipindi chote cha mchakato wa Ridhaa Huru, ya Awali na Inayofahamishwa ( FPIC), hasa katika hatua ya majadiliano. 3. Tengeneza mpango wa ufuatiliaji shirikishi na utatuzi wa migogoro, unaojumuisha utaratibu uliokubaliwa wa kuwawezesha wanajamii kuwasilisha malalamiko na kuhakikisha kuwa malalamiko hayo yanazingatiwa ipasavyo na kutatuliwa. ## Mahitaji kutoka kwa Kiwango cha Kilimo Endelevu Sehemu hii inatoa maelezo ya ziada kuhusu utekelezaji wa mahitaji mahususi na/au ya uboreshaji endelevu yanayotumika katika Kiwango cha Kilimo Endelevu (SAS) cha shirika la Rainforest Alliance. ## 3. Ramani za Hatari ya Ajira ya Watoto na Kazi ya Kulazimishwa **Zinazohusishwa na mahitaji ya uboreshaji endelevu 5.1.5, 5.1.6, 5.1.7 na 5.1.8** Mahitaji haya ya uboreshaji endelevu yanatumika pale ambapo kuna hatari ya wastani au kubwa ya ajira ya watoto na/au kazi ya kulazimishwa, kama inavyoonyeshwa katika ramani za hatari ya ajira ya watoto na kazi ya kulazimishwa za shirika la Rainforest Alliance. Ramani hizi za hatari huainisha kiwango cha hatari kwa nchi na sekta husika, na zinapatikana hapa: [https://www.rainforest-alliance.org/resource-item/data-sheet-for-child-labor-and-forced-labor-risk-maps/](https://knowledge.rainforest-alliance.org/docs/data-sheet-for-child-labor-and-forced-labor-risk-maps) Maelezo zaidi yametolewa kwenye ukurasa huu wa tovuti: [https://www.rainforest-alliance.org/in-the-field/manage-risk-with-the-rainforest-alliance-child-labor-and-forced-labor-sectoral-risk-maps/](https://www.rainforest-alliance.org/in-the-field/manage-risk-with-the-rainforest-alliance-child-labor-and-forced-labor-sectoral-risk-maps/) ## 4. Vigezo vinavyopendekezwa vya Mshahara wa Kujikimu kwa kila Nchi **Kinachohusishwa na hitaji mahususi 5.4.1** Vigezo vinavyopendekezwa vya Mshahara wa Kujikimu, (pamoja na thamani za marejeleo), vilivyotajwa katika hitaji la 5.4.1 la Kiwango cha Kilimo Endelevu cha shirika la Rainforest Alliance vinapatikana kupitia [Muungano wa Kimataifa wa Mshahara Unaokidhi Mahitaji ya Maisha (GLWC)](https://www.globallivingwage.org/). Wamiliki wa Vyeti wanaweza pia kutumia kigezo kingine chochote kinachotambulika kimataifa. Katika hali zote, usimamizi unahitaji kuhakikisha kuwa unatumia kigezo kilichosasishwa. Hiki kwa kawaida ndicho kigezo kinachopatikana katika mwaka wa kalenda uliotangulia. Kwa nchi zisizo na kigezo cha Mshahara wa Kujikimu, mshahara unaotumika kwa sasa unapaswa kutumika katika tathmini hadi pale kigezo hicho kitakapopatikana. Katika hali hii, mshahara unaopaswa kutumika ni ule wa chini uliowekwa kisheria au mshahara uliokubaliwa kupitia Mkataba wa Majadiliano ya Pamoja (CBA), kulingana na ule ulio juu zaidi, kwa kuzingatia hitaji la 5.3.3. > [!WARNING] > **Kumbuka:** Tathmini ya Mshahara wa Kujikimu haitumiki kwa mashamba madogo yaliyo chini ya uidhinishaji wa kikundi. ## Taarifa nyinginezo Tarehe ya kwanza ya kuchapishwa kwa hati hii (v 1.0): Julai 1, 2022. Nyaraka zilizotajwa kuwa *"zinazofunganisha"* lazima zizingatiwe ili kupata uthibitisho. Nyaraka zinazotajwa kama *"zisizo funganisha"* hutoa taarifa zisizo za lazima ili kuwasaidia wasomaji kuelewa na kutekeleza masharti pamoja na maudhui mengine yanayolazimisha. **Kanusho la Tafsiri** Kwa maswali yoyote yanayohusu maana sahihi ya taarifa katika tafsiri, rejelea toleo rasmi la Kiingereza kwa ufafanuzi. Makosa yoyote au tofauti za maana zinazotokana na tafsiri, hazilazishi na hazina athari kwa madhumuni ya ukaguzi au uthibitisho. Unakili, urekebishaji, usambazaji, au uchapishaji upya wa maudhui haya ni marufuku kabisa bila idhini ya maandishi ya awali kutoka kwa shirika la Rainforest Alliance. **Taarifa zaidi?** Kwa msaada wa kupata cheti cha shirika la Rainforest Alliance, wasiliana na timu yetu ya Mafanikio ya Wateja kupitia [customersuccess@ra.org](mailto:customersuccess@ra.org) Kwa taarifa zaidi kuhusu shirika la Rainforest Alliance, tembelea [http://www.rainforest-alliance.org](http://www.rainforest-alliance.org) wasiliana kupitia [info@ra.org](mailto:info@ra.org) au Ofisi ya shirika la Rainforest Alliance Amsterdam, De Ruijterkade 6, 1013AA Amsterdam, Uholanzi. **Futnodi** 1. Muda wa utekelezaji huanza kuhesabiwa kuanzia wakati malalamiko yanapopokelewa. [↑](/docs/social-annex-v13-swahili#footnote-ref-2) 2. Kamati ya Jinsia/mtu anayewajibika anahitajika kwa Wamiliki wa Vyeti vya Mashamba pekee, na lazima ashiriki katika mchakato wa kurekebisha ukiukaji wa mahitaji katika visa vya ukatili wa kijinsia na ubaguzi wa kijinsia. [↑](/docs/social-annex-v13-swahili#footnote-ref-3) 3. Ikiwa kisa kitatambuliwa na mkaguzi wakati wa ukaguzi, ushahidi kwamba marekebisho yamefanyika, uchambuzi wa chanzo kikuu cha tatizo umefanywa na hatua za kurekebisha zimepangwa, lazima uwasilishwe kwa shirika la uthibitishaji (CB) ndani ya wiki 10 baada ya siku ya mwisho ya ukaguzi (badala ya wiki 12). Kwa maelezo zaidi, tazama Kanuni za Uidhinishaji na Ukaguzi za shirika la Rainforest Alliance. [↑](/docs/social-annex-v13-swahili#footnote-ref-4) 4. Ikiwa kisa kitatambuliwa na mkaguzi wakati wa ukaguzi, mchakato mzima wa kurekebisha ukiukaji huo (hatua ya 4) lazima ukamilike kabla ya ukaguzi unaofuata, na ndani ya kipindi kisichozidi wiki 50 tangu siku ya mwisho ya ukaguzi uliotangulia (badala ya wiki 52). Ushahidi wa utekelezaji wa mpango wa hatua za kurekebisha na kuzuia kujirudia kwa ukiukaji lazima uwasilishwe kwa shirika la uidhinishaji (CB) angalau wiki 2 kabla ya ukaguzi unaofuata. Kwa maelezo zaidi, tazama Kanuni za Uidhinishaji na Ukaguzi za shirika la Rainforest Alliance. [↑](/docs/social-annex-v13-swahili#footnote-ref-5)